Saturday, November 30, 2013

MSAFARA WA MWENYEKITI UVCCM WAWEKEWA MAGOGO



Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB) Polisi mkoani Pwani inachunguza kundi la watu linalodaiwa kuweka magogo barabarani kuzuia msafara wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB) katika eneo la Tondoroni, wilayani Kisarawe, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema atazungumzia suala hilo baada ya kupata taarifa kamili.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, kundi hilo liliweka magogo hayo jana usiku katika barabara ya kati ya eneo la Mpuyani katika njia panda ya barabara iendayo vijijini kuingia barabara kuu ya Morogoro.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema katika nyakati tofauti kundi hilo lilianza kuzuia msafara huo kwa kutaka kushinikiza dai la mgogoro wa mipaka kati ya eneo la Jeshi la Wananchi wa Ulinzi Tanzania (JWTZ) na makazi ya watu katika eneo la Tondoroni, wilayani humo.
Watu hao ambao idadi yao haikuweza kufahamika walidaiwa kutishia kuchoma moto magari ya msafara huo wa mwenyekiti wakati alipotaka kushuka na kuzungumza nao na kuamua kujisalimisha kwa kuingia ndani ya gari na kurudi Kisarawe.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Tanzania Visiwani mapema akiwahutubia wananchi wa Kisarawe aliwataka kudumisha amani kwa kukiweka Chama Cha Mapinduzi madarakani. “Amani ikivurugika hakuna atakayekuwa salama, hata askari nao hawatokuwa salama”.
Akiongea na viongozi wa CCM na UVCCM katika jengo la ofisi za CCM wilaya, aliwataka wanachama hao kuvunja makundi ya kampeni kwa kuwa hayana tija kwa sasa, isipokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Alisema kuwa Muungano wa Tanzania ni muhimu hivyo changamoto zilizomo ndani yake zitafutiwe muafaka kwa njia ya amani.
Alisema kuna baadhi ya watu wakorofi ambao wanadai muungano uvunjwe hasa kutoka Pemba wakidai kuwa kisiwa hicho ni chao wakati visiwa hivyo vya Pemba na Zanzibar havina wenyewe na watu walioko huko wametokana na biashara ya utumwa na wengi wao walitoka upande wa Tanzania Bara wa makabila mbalimbali.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alimsimika mwandishi wa siku nyingi, Abubakar Mlawa kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na wengine 15 wakiwamo madiwani kuwa makamanda wa UVCCM wa kata zao.


CHANZO: NIPASHE

Tags:

0 Responses to “MSAFARA WA MWENYEKITI UVCCM WAWEKEWA MAGOGO”

Post a Comment

Ila tafadhali sana angalia usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu.

HHHHHHHHHHHH

Subscribe

Kwa habari na Taarifa weka Email yako Hapa tutakutumia

© 2014 FUNUNU HABARI.. All rights reserved.
Designed by FUNUNU HABARI