Tuesday, June 11, 2013

ROBIN VAN PERSIE APANIA KUFIKIA REKODI ZA THIERRY HENRY NA ALAN SHEARER



Mshambuliaji hatari kutoka Uholanzi anaekipiga Man U, Robin van Persie amedhamiria kutwaa kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora kwa mara ya tatu mfululizo na kuungana na Thierry Henry na Alan Shearer waliowahi kufanya hivyo.

Wakati Shearer alifanya hivyo 1994–95 (mabao 42), 1995–96 (mabao 35) akiwa na Blackburn Rovers na 1996–97 (mabao 31) akiwa na Newcastle United, Henry alifuatia 2003–04 (mabao 37), 2004–05 (mabao 32) na 2005–06 (mabao 32) mara zote akiichezea Arsenal.

Mbali na hilo, mkali huyo wa Uholanzi pia alipeleka ujumbe kwa kocha wake mpya David Moyes akisema kuwa ni lazima mataji yaendelee kumiminika kwa kuwa United ni timu yenye viwango.

Van Persie aliibuka na kiatu cha dhahabu kwa mara ya pili mwaka huu akipachika mabao 26 katika msimu wake wa kwanza akiwa na United.

Mara ya kwanza aliibuka kinara wa mabao mwaka 2012 wakati alipoiaga Arsenal kwa kufunga mabao 30 kabla ya kuhamia United kwa dau la pauni milioni 24 kiangazi kilichopita.

Licha ya kustaafu Sir Alex Ferguson, staa huyo anaamini United itaweza kuendeleza mafanikio yake chini ya kocha mpya Moyes, huku naye akizidi ‘kuchana nyavu’ za wapinzani.

“Nina hisia kwamba tunaweza kufanya mengi zaidi, na kwamba tunaweza kushinda mataji mengi zaidi,” alisema van Persie.

United watakabiliwa na changamoto mpya kutoka Chelsea na Manchester City, huku timu zote tatu zikianza maisha chini ya makocha wapya.

Lakini Van Persie amebaki na ujasiri kwamba taji la Premier League litabaki Old Trafford.

“Tunakwenda kwenye zama mpya, changamoto mpya, na kocha mpya, labda pia baadhi ya wachezaji wapya watakuja na wengine wataondoka, hakuna anayejua.

“Lakini kila mmoja anajua viwango vyetu. Tunataka kushinda ligi tena,” alisema.



Tags:

0 Responses to “ROBIN VAN PERSIE APANIA KUFIKIA REKODI ZA THIERRY HENRY NA ALAN SHEARER ”

Post a Comment

Ila tafadhali sana angalia usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu.

HHHHHHHHHHHH

Subscribe

Kwa habari na Taarifa weka Email yako Hapa tutakutumia

© 2014 FUNUNU HABARI.. All rights reserved.
Designed by FUNUNU HABARI