Friday, June 28, 2013

Kaseja na shukrani ya punda…





HABARI za kushitua katika soka ya Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla ni kutemwa kwa kipa namba moja wa Simba na Tanzania, Juma Kaseja.




Ni habari za kushtusha kwa sababu naamini hakuna aliyetarajia hilo kutokea kwa kipa huyu ‘Tanzania One’ kutemwa akiwa yuko kwenye kiwango chake cha hali ya juu. Taarifa hizo zinanikumbusha usemi wa tenda wema wende zako usingoje shukrani, ama shukrani ya punda mateke, ndivyo inavyotokea kwa kipa huyu.

Hakuna asiyefahamu umahiri wa Kaseja langoni, ndio maana taarifa za kutemwa kwake Simba hazikuwashtua mashabiki na wapenzi wa soka wa Tanzania pekee, bali naamini hali hiyo pia ipo hata Afrika Mashariki na Kati kwani kote huko wanaijua ‘shughuli’ ya kipa huyu aliyesajiliwa Simba akitokea Moro United ya Morogoro wakati huo mwishoni mwa mwaka 2002.

Binafsi mpaka sasa sijajua sababu ya Simba kumtema Kaseja, kwani Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Ismail Aden Rage hataki kuweka wazi sababu za kutomsajili tena mchezaji huyo. Hata Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspoppe pia haweki wazi sababu za kumtema kipa huyo, zaidi ya kusema tu kwamba hayo ni maamuzi ya Kamati ya Utendaji yaliyofikiwa katika kikao chake kilichokutana mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Hakuna mazungumzo yaliyofanywa na Kaseja, tumeamua kwamba hatuendelei tena, ndio hivyo,” alisema Hanspoppe kwenye kituo kimoja cha redio juzi. Kuna taarifa zinadai kwamba Simba wamemuacha Kaseja kwa sababu anataka Sh milioni 50 ili apewe mkataba mpya, taarifa ambazo mhusika mwenyewe Kaseja anazikanusha kwamba hata kukaa meza moja na Simba kuzungumzia suala la usajili hawajakaa.

Ukisikiliza kwa makini kauli ya Mwenyekiti Rage na Hanspoppe utagundua Simba hawana sababu yoyote ya kumtema Kaseja na hapo ndipo linapokuja suala la chuki binafsi kwa maslahi ya watu fulanifulani.

Na kwa vile hawakuwa na sababu za msingi za kumtema Kaseja ndio maana uamuzi wa kubaki ama asibaki ukafanyika kwa kupiga kura, bila aibu klabu hiyo kubwa miongoni mwa klabu za Afrika Mashariki na Kati ikafanya uamuzi wa kumsajili mchezaji kwa kupiga kura.

Kizamani kabisa! Halafu Kamati ya Utendaji ndio inayosajili ama Kamati ya Ufundi ndio yenye jukumu hilo? Hiyo ni kazi ya Kamati ya Ufundi si ya Utendaji, lakini kwa wenzetu hawa wameamua kupoka majukumu ya kamati hiyo. Lakini, inawezekana kabisa Simba hawamtaki Kaseja iwe kwa kiwango kushuka ama kwa maslahi ya watu fulanifulani ndani ya timu hiyo, iwe iwavyo, hawakustahili kumuacha kihuni kipa huyo.

Kaseja amekaa Simba takribani miaka kumi, hastahili kuondolewa kama mchezaji ambaye ameifanyia mabaya klabu hiyo. Simba na klabu nyingine wajifunze kulipa fadhila, neno fadhila sio mpaka iwe fedha ama kitu cha thamani, kitendo cha kumfanyia mtu ustaarabu ni fadhila tosha. Kwa nini klabu zetu hazijifunzi ustaarabu kama nyingine?

Mfano wa juzi tu, Barcelona ya Hispania imemuacha Erick Abidal kistaarabu na mkutano na waandishi wa habari kaitwa akazungumza na viongozi wake, wachezaji wenzake wakazungumza na kuagana kwa amani na upendo. Sasa mchezaji huyo anajiandaa kucheza Ufaransa. Hata leo, hii akielezwa arudi kwa kazi nyingine, anaweza kufanya hivyo bila kinyongo.

Halafu Simba huwa haijifunzi, ilimfanyia ‘umafia’ unaofanana na huo beki wake wa kati mkali enzi hizo, Boniface Pawasa. Ilimuacha akiwa kwenye kiwango chake cha hali ya juu na yeye kama ilivyo kwa Kaseja, timu za Tanzania na Afrika Mashariki na Kati zote zilikuwa zikifahamu ‘shughuli yake’.

Lakini Pawasa aliachwa, kisa tu watu wachache wenye maslahi yao walimtuhumu kuhujumu timu. Pawasa akaondoka na umahiri wake, Simba haikujali mchango wake.

Sasa hili la Pawasa limekuja kwa Kaseja. Inadaiwa kwenye kikao hicho cha Kamati ya Utendaji wahusika walivutana katika usajili wake, mwisho wakafikia tamati wapige kura, waliosema aondoke wakawazidi wachache wanaotambua mchango, utu na thamani ya kipa huyo waliosema asiondoke.

Mimi nadhani Simba kuna tatizo, tena si dogo ndio maana hata usajili wake misimu miwili iliyopita umekuwa wa kuungaunga, haueleweki. Kwa Kamati ya Usajili, Kamati ya Utendaji, Kamati ya Ufundi makini, si kazi rahisi kumuacha kipa Kaseja.

Wakati Simba inaanza mazoezi chini ya kocha wake mpya Abdallah Kibadeni kwenye Uwanja wa Kinesi, liliibuka kundi la wanaojiita wanachama wa Simba wakimzonga kocha kwamba asimtumie kipa huyo na hawataki asajiliwe kwani kiwango chake kimeshuka.

Yaani hao mashabiki wa Simba waliokuwa hawamtaki Kaseja, walisahau walivyotaabika alipokwenda Yanga? Wanadharau nazi wakati embe tunda la msimu? Wameamua kutema Big G kwa karanga za kuonjeshwa? Najiuliza kiwango cha Kaseja kimeshuka vipi? Kaseja anaweza kuwa bora kuliko makipa wengine pale Simba akiwemo Abel Dhaira.

Kama hivyo sivyo, kipi kilimfanya Kocha Patrick Liewig na hata mtangulizi wake, Milovan Circkovic kwa nini hawakuwa wakimpa namba? Hapo ipo namna. Naamini Simba siku si nyingi watamkumbuka Kaseja, kama walivyomkumbuka Pawasa wakati fulani, Nurdin Bakari, na sasa Kelvin Yondani anayecheza Yanga bila wasiwasi wowote licha ya maneno ya karaha aliyotolewa kutoka Simba.

NA-HABARI LEO.

Tags:

0 Responses to “Kaseja na shukrani ya punda…”

Post a Comment

Ila tafadhali sana angalia usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu.

HHHHHHHHHHHH

Subscribe

Kwa habari na Taarifa weka Email yako Hapa tutakutumia

© 2014 FUNUNU HABARI.. All rights reserved.
Designed by FUNUNU HABARI