Sunday, December 1, 2013
Matawi 189 ya CHADEMA jijini mwanza yatishia kuandamana endapo Mbowe na Dr. Slaa hawatajiuzulu kabla ya tarehe 4 disemba na endapo watakanyaga Mwanza basi watawapiga mawe
TAMKO LA UMOJA WA MATAWI YA WANACHADEMA MKOA WA MWANZA DHIDI YA UAMUZI HARAMU WA KAMATI KUU YA CHADEMA.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTANGULIZI
Ndugu
wanahabari, mbele yenu ni muunganiko wa wawakilishi wa matawi 189 ya
chama cha demokrasia na maendeleo mkoa wa mwanza. Umoja huu wa matawi
unawajumuisha wajumbe kutoka majimbo yote ya mkoa wa mwanza.
Hivyo
katika kikao chetu tulichoketi tarehe 30.nov 2013 kuanzia saa nne
asubuhi mpaka saa tisa kasorobo, pamoja na mambo mengine tumeazimia
kuanzisha umoja huu wa wanachama.
Hii
ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu wanaotuwakilisha kwenye
vikao vya maamuzi kama vile wilaya, mkoa na taifa wamekuwa waoga na
wameshindwa kuwakilisha mawazo yetu tuliyowatuma badala yake wengi wao
wamekubali kuwa vibaraka wa kile kinachoitwa CHADEMA KASKAZ
Kutokana
na ukweli kwamba msingi wa chama chetu na chama kingine chochote kile
cha siasa, uimara na uhai wake unatokana na uwepo wa misingi na matawi
ya chama, hivyo sisi wanachama wa matawi haya 189 tumeamua kuunganisha
nguvu zetu kutetea chama chetu na kuhakikisha haki, heshima, katiba na
maadili ya chama vinafuatwa bila ya kuogopana wala kuoneana haya.
Umoja huu umeonelea ni vyema kuutaarifu umma wa watanzania na wapenzi na wanachama wa chadema mambo kadhaa yafuatayo
Kwamba:-
Chadema
ni chama cha siasa kinachopaswa kuendeshwa kwa misingi ya kufuata
taratibu, kanuni na katiba yake na si vinginevyo. Lakini badala yake
kwasasa kumeibuka ombwe kubwa kwa viongozi wetu wa juu kujitwalia
mamlaka ya chama kinyume na matakwa ya katiba ya chama chetu hususan
katika kutoa haki sawa kwa viongozi na wanachama wa chama chetu.
Kumekuwepo
na upendeleo wa hali ya juu sana kwa wale wanao amini kuwa ndani ya
chama hawawaungi mkono hivyo kupelekea kuwaadhibu kama ndio kinga yao ya
kuendelea kuongoza bila kuhojiwa au kukosolewa.
Sababu zilizotolewa na kamati kuu hazikubaliki
Maamuzi
ya kamati kuu ya tarehe 20-21 /11/2013 ya kuwavua uongozi Mh: Zitto
Zuberi Kabwe, Dr. Kitila Mkumbo na Ndg Samson Mwigamba, kumeonyesha
dhahiri si woga tu wa Demokrasia bali ni unafki na Uzandiki wa hali ya
juu sana kwa viongozi wetu kuikwepa Demokrasia kwa kisingizio cha
kusaliti na uhaini ndani ya chama.
Katiba
yetu imeweka wazi Ibara ya 6 Kifungu cha 3 kipengele cha 6. (a – f)
Mamlaka za nidhamu na uwajibishaji ndani ya chama. Kulikuwa na haraka
gani ya kufanya maamuzi bila kufuata taratibu hizi kwa viongozi hawa?
Tuonavyo
sisi baadhi ya wanachama huo ni umangi meza na udhalilishaji wa
kibaguzi ndani ya chama kwa viongozi wetu waliotumia nguvu zao na akili
nyingi sana kukijenga chama.
Sababu kubwa ya kuandamwa kwa viongozi hawa ni
1. Kutaka kujua mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na Ruzuku ya fedha za serikali.
2. Michango ya wanachama na wapenzi kwenye mikutano ya wazi.
3. Harambee za M4C Mwanza, Arusha na Dar es saalam.
4.
Kutaka kujua taratibu za manunuzi ya rasilimali ya chama namna
walivyopatikana wazabuni wa kusambaza bendera na kadi za chama, magari
na pikipiki ambapo ununuzi wake ni wa mashaka makubwa.
5.
Kutaka kuona usawa wa kimadaraka kwa viongozi wote bila ubaguzi wa aina
yoyote kuanzia ngazi ya chini mpaka Taifa kinyume na ilivyo sasa hasa
makao makuu ya chama ambapo ukanda na ubaguzi wa hali ya juu umetawala.
Kushamiri kwa migogoro
Mwenyekiti
na katibu mkuu wameshindwa kutatua migogoro ya viongozi na wanachama
kutoka mikoani kwa njia sahihi za vikao na kwa wakati hivyo kutoa mwanya
kwa viongozi na wanachama kutumia njia ya mitandao ya kijamii
tukiongozwa na katibu mkuu mwenyewe kujitokeza mara kwa mara kwenye
mitandao hiyo hiyo kwa madai ya kutolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali
yahusuyo maswala ya chama ilihali akijua kufanya hivyo ni usaliti mkubwa
kwa chama chake.
Njia
hiyo ya nje ya vikao ilipelekea migogoro mikubwa sana hususan mkoa wetu
wa Mwanza na kupelekea kupoteza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutokana
na kufukuzwa kwa baadhi ya madiwani, kuvunjwa uongozi wa mkoa na wabunge
kuwa juu ya chama na kutumia nafasi zao kupanga safu za uongozi wanao
uona watawatumikia wao na si chama hivyo kusababisha mifarakano mikubwa
ndani ya chama na kupelekea kuvuliwa uongozi kwa viongozi mbalimbali
katika mkoa wetu kwa maamuzi yasiyo zingatia utafiti na uhalisia wa
kweli ndani ya chama.
Mwenyekiti na katibu mkuu wamekuwa vinara wa kuvunja katiba Mfano:
Kitendo
cha kutoa muongozo nje na matakwa ya katiba juu ya kuwapata wawakilishi
kwenye vyombo vya maamuzi kama wabunge kwamba wanaohitaji kugombea 2015
waandike barua makao makuu na wao ndio watatoa wagombea kinyume na
katiba ya chama Ibara 7.2.13 inayotoa taratibu ya kuwapata wagombea.
Huo ni uvunjaji wa katiba na ubakaji wa demekrasia ndani ya chama. Sidhani kama kuna uhaini zaidi ya huu .Swali la kujiuliza hapa,
Je, kama leo sisi Chadema hatuheshimu katiba yetu tuliyoitunga sisi
wenyewe itakuwaje siku tukikabidhiwa nchi yenye watu wenye mawazo na
mtizamo tofauti na sisi?. Hatutaki kuamini kama nchi hii inaweza kugeuka uwanja wa maopambano ya kivita.
Tunataka
kujua hatua gani zilizochukualiwa dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini Mh:
Godbless Lema kumkashfu kiongozi wa chama Mh: Zitto Zuberi Kabwe kuwa ni
mnafiki na Mzandiki kwenye mitandao ya kijamii .
Pia
tunataka kujua hatua gani zilizochukuliwa na chama dhidi ya Bw Henry
Kilewo kwa kuweka waraka unaoitwa ripoti ya siri inayomhusu Zitto.
Chadema
makao makuu kupitia kwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama ilikana
mbele ya vyombo vya habari kuwa haihusiki na waraka huo , lakini Bw
Kilewo ambaye pia ni kiongozi wa chama ngazi ya mkoa wa Kinondoni
aliuweka waraka huo kwenye Blog yake ilihali akijua kufanya hivyo ni
kinyume na kanuni za viongozi wa chama kuhusu maadili ya viongozi kanuni
ya 10.
Tunataka
kuona nguvu iliyotumika kuwaadhibu Mh: Zitto na wenzake kwa kuandaa
waraka ujulikanao kama mkakati wa mabadiliko 2013 inatumika kwa hawa
waliotumia njia chafu ya kuandaa waraka wa kumchafua zitto ambao chama
kinawajua na baadhi yao tumewaweka humu kwenye tamko letu.
Matwakwa yetu:
1.Mwekiti
na katibu mkuu wajiuzulu mara moja ili kupisha uchunguzi wa mapato na
matumizi ya fedha za chama ambazo zinatokana na kodi za wavuja jasho
wananchi .
2.M/kiti
na katibu mkuu watoe ufafanuzi juu ya kuvunja katiba kwa kuondoa
kipengele cha ukomo wa uongozi ndani ya chama .Kutangaza uchaguzi huku
mkiwaondoa washindani wenu ni uwoga na ubakaji wa Demokrasia.
Hitimisho:
Tunataka
maamuzi haya HARAMU yaliyofanywa na kamati kuu yabatilishwe na mchakato
wa kuwavua viongozi hawa nyazifa zao ufuate taratibu na kanuni kwa
mujibu wa katiba.
Tofauti na hapo tarehe 4/12/2013 tutaungana na wapigania Demokrasia kote nchini kufanya maandamano yasiyokuwa na ukomo mpaka uongozi uliopo utoke madarakani.
Baada ya tarehe hiyo tunataka mhakikishe mnawahamisha wabunge vibaraka wote wa chadema mkoa wa mwanza.
Mchukueni
Wenje mkamtafutie jimbo Moshi na Highness Kiwia mkamtafutie jimbo HAI
na MACHAME.Hii ardhi ya kanda ya ziwa sio saizi yao na tunataka waondoke
mara moja. Kinyume na hapo tutawaondoa huku wakishuhudia kwa macho yao.
Pia
tunamuagiza Mbowe na Slaa wasithubutu kukanyaga ardhi hii ya kanda ya
ziwa ikiwa bado hawajajiuzulu ama kubadili maamuzi yao HARAMU haraka
iwezekanavyo. Hatuna sababu ya kuendelea kuwa watumwa wa fikra ndani ya
chama chetu.
ROBERT E. GWANCHELE
Mwenyekiti wa umoja wa Matawi ya CHADEMA mkoa wa MWANZA
Mwenyekiti wa Vijana KANDA YA CHAMA ZIWA MAGHARIBI
Mjumbe kamati Tendaji wilaya ya ILEMELA

This post was written by: Author Name
Author description goes here. Author description goes here. Follow him on Twitter
Get Updates
Subscribe to our e-mail newsletter to receive updates.
0 Responses to “Matawi 189 ya CHADEMA jijini mwanza yatishia kuandamana endapo Mbowe na Dr. Slaa hawatajiuzulu kabla ya tarehe 4 disemba na endapo watakanyaga Mwanza basi watawapiga mawe”
Post a Comment
Ila tafadhali sana angalia usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu.